Image result for TFF JAMALI MALINZIRAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema watafanya marekebisho ya kanuni zao za soka ili ziendane na zile za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kupata mshindi ‘halali’ pale timu zinapofungana pointi.
Malinzi alisema hayo jana wakati akitoa shukrani kwa Rais John Magufuli na Serikali yake na Watanzania kwa kuiunga mkono timu ya Taifa ya Vijana walio chini ya miaka 17 ‘Serengeti boys’ iliyoshiriki fainali za 12 za Vijana zilizofanyika Gabon Mei 14-28 na kutolewa kwa kanuni.
Alisema Serengeti Boys iliondolewa hatua ya makundi kwa kipengele cha kuangalia mechi na mpinzani mliyefungana naye pointi nani alimfunga mwingine akaahidi kubadili kanuni za TFF ziwe kama za CAF.
“Kanuni iliyotumika kuiondoa Serengeti Boys kwenye mashindano tungekuwa tunaitumia kwetu basi Simba angekuwa bingwa Ligi Kuu msimu wa 2016/2017,” alisema. Katika mechi kati ya Simba na Yanga, Simba ilishinda kwa mabao 2-1 lakini Yanga ilitwaa ubingwa kutokana na kuwa na mabao mengi ya kufunga na kufungwa.
Simba wamelalamikia ubingwa huo kwa barua Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wakipinga kupokwa pointi mechi na Kagera Sugar ambayo walidai kuwa ilichezesha mchezaji mwenye kadi tatu za njano.
Endapo TFF ilikuwa inatumia kanuni hiyo, basi Simba ingekuwa bingwa kwani baada ya ligi kumalizika Simba na Yanga zilikuwa sawa kwa pointi 68 lakini ingefaidika kwani mchezo wa awali ilitoka sare ya 1-1.
Raundi ya pili Simba ilishinda mabao 2-0. Malinzi alisema anaamini Kamati ya Utendaji itakubali kupitisha kipengele hicho ili kuanzia msimu ujao, kanuni hizo zitumike kwenye ligi zote za TFF.
Malinzi alisema watashusha mashindano ya U-20 kuwa ya wachezaji wa U-17 ili kupata timu za vijana imara wanaotokea katika klabu kuliko ilivyo sasa TFF ndio yenye jukumu la kuandaa timu za vijana. Serengeti Boys katika mashindano ya AFCON U-17 ilikuwa kundi B na Mali, Angola na Niger.
Iliondolewa na Niger. Katika mchezo wa awali, Serengeti boys ilitoka suluhu na Mali, ikaifunga Angola mabao 2-1 na kufungwa na Niger bao 1-0. Malinzi alisema Serengeti Boys sasa itakuwa ndio U-20, ‘Ngorongoro Heroes’ ambayo itacheza fainali za Afrika za U-20 zitakazofanyika nchini 2019 hivyo makocha wataanza kambi kuiandaa kwa mechi za majaribio ndani na nje ya nchi. Pia Malinzi aliipongeza U -20 ya Zambia kwa kufuzu robo fainali ya mashindano ya Vijana ya dunia ya U-20 Korea Kusini.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top