Image result for DK RUGEMELEZA NSHALA
MKURUGENZI Mtendaji wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), Dk Rugemeleza Nshala, amevunja ukimya na kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuhakikisha nchi inanufaika na mikataba ya madini.
Akizungumza katika mahojiano maalumu katika kipindi cha Semakweli kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel 10 juzi juu ya mada iliyohusu “Makinikia- Tulifikaje na Tutatokaje Kisheria,” Dk Nshala alisema hatua za Rais Magufuli kufanya ukaguzi wa mchanga wa dhahabu ni sahihi kisheria.
“Nchi yetu ina haki ya kufanya ukaguzi au uchunguzi wa mali zake kwani ina umiliki wa milele wa rasilimali zake hivyo ina haki ya kujiridhisha kwa kile kinachoendelea na kilichomo ndani ya makontena yale,” alisema Dk Nshala.
Alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu mshirika wake wa zamani, waliyefanya naye kazi katika taasisi ya LEAT, Tundu Lissu asikike akikosoa hatua zilizochukuliwa na Rais Magufuli.
Dk Nshala pia alizungumzia wasiwasi wa Tanzania kushitakiwa kimataifa, akisisitiza kuwa mpaka sasa hajaona jambo la kutia hofu hiyo, ingawa ameitaka serikali kuhakikisha inachukua kila hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za kimkataba.
Alisema pia hakubaliani na dhana kwamba mikataba hiyo haiwezi kuguswa, akitoa mifano ya nchi mbalimbali ambako baada ya haki kubadilika mikataba ya madini hupitiwa upya kwa faida ya pande zote mbili.
“Sijaona tatizo serikali kujiridhisha kwanza na undani wa kile kinachosafirishwa nje labda kama ingechukua hatua hizo bila kufuuata sheria. Mkataba wowote unaweza kupitiwa hasa kunapobainika mabadiliko ya hali iliyokuwepo wakati wa kusaini mkataba huo.
Ni juu ya Serikali sasa kutoa notisi ya mazungumzo kurekebisha mikataba,” alisema. Aliikumbusha serikali kuhakikisha inafuata kila hatua za kisheria katika suala la mchanga, hata pale inapobaini kuwa imeibiwa, kwani wawekezaji wengi wanakinga katika mifumo ya kisheria ya kimataifa.
“Wawekezaji wanapokuja nchini hawaji hivi hivi wanakuja na bima za kimataifa za kiuwekezaji kama kinga ya kisiasa ili iweze kuwasaidia endapo Serikali husika ikipingana nao, lakini suala la kudai kujadiliwa upya kwa mkataba ni haki ya nchi,” alisema Dk. Nshala.
Mbali na hayo, Dk Nshala aliishauri serikali kukagua kampuni zote za madini nchini zaidi ya Acacia ili kupata picha zaidi ya namna madini yetu yanavyoibiwa au kutoroshwa nje ya nchi.
Vilevile, aliishauri serikali kukaguliwa upya mikataba ya madini na kutungwa sheria nzuri zaidi na kulipa Bunge mamlaka ya kujadili na kupitia mikataba hiyo kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Dk Nshala amebobea katika taaluma za sheria hasa za mazingira na masuala ya madini, akiwa ni mmoja wa Watanzania wachache waliosoma ngazi ya shahada ya uzamili (Masters) na shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu mashuhuri zaidi duniani cha Harvard (Harvard School of Laws) kilichopo nchini Marekani.

Hivi karibuni Rais John Magufuli alipokea ripoti ya uchunguzi wa mchanga kwenye makontena 277 ambapo Kamati yake imebaini kuwepo kwa viwango vingi vya juu vya madini ya dhahabu, shaba, chuma na mengine ndani ya mchanga huo.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top