Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema atachukua hatua kwa kitendo cha kusukumwa kilichofanywa na askari wa Bunge mwishoni mwa wiki.
Alisema atafanya hivyo mara baada ya kumaliza msiba wa mmoja wa waasisi wa chama hicho, Philemon Ndesamburo.
“Nitatoa tamko na kuchukua hatua nikimaliza msiba, leo (jana) na kesho (leo) nipo msibani huku Moshi, lakini nitafafanua na kuzungumzia hilo nikimaliza,” alisema.
Mnyika alitolewa bungeni kwa nguvu na askari wa Bunge baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwaamuru kumtoa ndani akidaiwa kukiuka kanuni za Bunge wakati akichangia mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia, mbunge huyo alipewa adhabu ya kutohudhuria vikao saba vya Bunge, huku askari hao wakimtoa ndani kwa nguvu na kumsukuma.
Ndesamburo, ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Moshi Mjini kwa miaka 15 mfululizo ataagwa leo katika Uwanja wa Majengo mjini Moshi na baadaye mwili wake utapelekwa nyumbani kwake ambako taratibu za mazishi zitafanyika kesho.
Wakati Mnyika akisubiri kumzika Ndesamburo, Chadema Wilaya ya Ubungo imelaani kitendo alichofanyiwa mbunge huyo ikisema hakikuwa cha kiungwana na kilikiuka hadhi yake.
Katibu Mwenezi wa Chadema wilayani humo, Perfect Mwasiwelwa alisema kitendo alichofanyiwa Mnyika kingeweza kumletea majeraha kama angeanguka kutokana na mazingira ya eneo aliposukumiwa.
Mwasiwelwa alisema mwanasiasa huyo anawawakilisha wananchi zaidi ya 78,000 hivyo Chadema inalaani kitendo hicho kwa sababu si cha utu.
“Alitolewa nje katika mazingira ambayo sio ya utu, sio ya Kitanzania, sisi kama chama ngazi ya wilaya tunasema hakikuwa kitendo cha kawaida kabisa,” alisema.
Wakati huo huo, wabunge wawili wa Chadema; Halima Mdee (Kawe) na Esther Bulaya (Bunda Mjini) leo watasomewa hukumu yao baada ya Kamati ya Kudumu ya Maadili ya Bunge kuwajadili na kumshauri Ndugai hatua sahihi za kuwachukulia.
Chapisha Maoni