Makubwa Haya!! Wananchi wa Kitongoji cha Bujinge,kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi manispaa ya Shinyanga wamejikuta katika wakati mgumu baada ya kuchimba kaburi kisha kulazimika kufukia kaburi hilo la mtoto aliyedaiwa kufariki dunia.


Malunde1 blog imezungumza na mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo,Salum Juma,anasimulia ilivyokuwa:

“Kuna mama mmoja anaitwa Suzana Charles kwao ni Kizumbi lakini ameolewa huko Musoma,aliondoka Shinyanga akiwa na mtoto aliyezaa na mwanamme mwingine,juzi kapiga simu kwenye nyumbani kwao Kizumbi kuwa mtoto wake amefariki,na wanasafirisha mwili wa marehemu kutoka Musoma hadi Shinyanga,kama zilivyo taratibu za wananzengo tukaanza taratibu za kushughulika na msiba”,anaeleza Salum Juma.

“Jana tulihudhuria msibani nyumbani kwa marehemu Mzee Charles hapa Kizumbi,tukachimba kaburi,tukawa tunawasiliana naye akisema wapo njiani wanakuja,baadaye huyo mama akasema wamefika Misungwi Mwanza lakini gari yao imemaliza mafuta hivyo tuwatumie pesa,tukawatumia shilingi laki moja na simu yake haikuwa inapatikana tena”,anasimulia Juma.

“Baada ya kutuma shilingi laki moja,tukategemea kuwa safari inaendelea,tukaendelea na taratibu za mazishi tukiamiani kuwa mpaka saa tisa alasiri watakuwa wamefika Shinyanga,huwezi amini mpaka saa 12 walikuwa bado hawajafika,tukakubaliana kuwa kesho yake yaani leo tufike kwa ajili ya kuendelea na msiba”,

“Ilipofika saa nne usiku jana,Yule bwana aliyekuwa amemuoa huyo mwanamke akapiga simu anauliza mke wake kama amefika Shinyanga? Maana ametoka Musoma,tukamuuliza kuhusu msiba,akasema hana taarifa za msiba kwani mke wake ametoroka na mtoto akiwa salama”,

“Leo tumeamka tukaambiwa kuwa hakuna msiba wowote,hivyo nzengo tumedanganywa,na kaburi letu tulikuwa hatujalifukia tunaendelea kujadili,kidogo majira ya saa nne asubuhi leo Jumapili Yule mama akawa amewasili Kizumbi,Shinyanga akiwa na mwanae,amefika hapa kwao,tumempokea,tukaanza kumhoji kuhusu kilichotokea”,


“Tulipomhoji amesema ameamua kufanya hivyo kutokana na matatizo ya kifamilia kule alikokuwa anasumbuliwa na maradhi hana pesa ya kumsaidia kupata matibabu,imefikia hivyo na sasa ndiyo tumemaliza kufukia kaburi”,anaeleza Salum Juma.
Imeandaliwa na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top