Wataalamu wa mambo ya kale wamegundua mabaki ya mji wa kale ambao ulikuwa umesahaulika mashariki mwa Ethiopia.
Wanaakiolojia hao wanakadiria kwamba mji huo ulikuwepo kuanzia karne ya 10 na ulikuwa kitovu cha biashara katika eneo hilo.
Kugunduliwa kwa mabaki ya mji huo wa Harlaa kumefichua kuwepo kwa vitu, bidhaa na vifaa kutoka maeneo ya mbali kama vile Misri, India na China.
Miongoni mwa vitu vilivyogunduliwa eneo hilo ni msikiti ambao inakadiriwa ulijengwa karne ya 12, pamoja na makaburi ambayo yalitumiwa na Waislamu waliokuwa wanaishi eneo hilo.
Mwanaakiolojia mkuu anasema muundo wa msikiti huo unafanana sana na misikiti iliyogunduliwa kusini mwa Tanzania na maeneo ya Somaliland, na ni ishara wkamba kulikuwa na uhusiano na mawasiliano kati ya jamii za Waislamu barani Afrika.Wataalamu hao pia wamegundua sarafu za fedha na shaba za karne ya 13 kutoka Misri, pamoja na vito kutoka Madagascar, Maldives, yemen na China.
Wakulima katika eneo hilo wamekuwa wakipata vitu vya ajabu, vikiwemo sarafu kutoka China katika mashamba yao, jambo ambalo lilichangia kuenea kwa dhana kwamba eneo hilo huenda lilikuwa makao ya majitu.
Wanakiolojia hao hata hivyo wanasema hawakupata ushahidi wowote kwamba kulikuwa na majitu eneo hilo.
Watachimbua zaidi na kutafiti katika eneo hilo katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Watachunguza pia mabaki ya miili ya watu 300 iliyozikwa katika makaburi yaliyogunduliwa, kubaini walikuwa wanakula nini walipokuwa hai.Vitu vilivofukuliwa kutoka eneo hilo vitawekwa katika kituo cha turathi eneo hilo na katika makavazi ya taifa mjini Addis Ababa.
Chapisha Maoni