WABUNGE wanaotoka maeneo ya wafugaji na wakulima wametunishiana misuli kwa kurushiana maneno bungeni jana Bunge hilo lilipokaa kama Kamati ya Matumizi kwa ajili ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2017/18.
Utulivu ndani ya Bunge hilo ulivurugika pale Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) alipotoa hoja ya kutoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwa kuwa hakumpatia majibu mazuri kuhusu hoja ya kuonewa kwa wafugaji. Kwa mujibu wa utaratibu wa kamati hiyo ya matumizi, mbunge anapotoa hoja ya kushika shilingi, wabunge wanaomuunga mkono na wanaomuunga mkono waziri hupewa nafasi ya kuchangia ili hoja husika ipatiwe ufumbuzi.
Hata hivyo, hoja hiyo ya Msukuma iliibua mjadala kutokana na wabunge wengi kumuunga mkono kutetea wafugaji huku waliokuwa wakimuunga mkono Waziri Maghembe wakikataa kushindwa wakitetea wakulima. Akiwasilisha hoja yake, bungeni hapo, Msukuma alitaka Waziri huyo atoe majibu kuhusu uonevu unaoendelea mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako maofisa wa maliasili wamekuwa wakipiga minada mifugo wanayoikamata.
“Nilisema nitashika shilingi ya waziri kama hatatoa majibu ya niliyouliza hususani uonevu wa watu wa maliasili unaoendelea kwenye maeneo yetu ya Kanda Ziwa. Lakini hapa tunavyoongea leo, tayari nina taarifa kuwa ng’ombe 1,200 wanapigwa mnada jimboni kwangu,” alisema Msukuma. Aliungwa mkono na mbunge wa Serengeti, Chacha Rioba (Chadema) aliyesema kinachoendelea kati ya wafugaji na maaskari wa hifadhi ni rushwa. “Hii ni biashara ya wafugaji na askari. Wewe na wizara muangalie utaratibu wa kudhibiti wakati migogoro ya ardhi likishughulikiwa,” alisema.
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) alitaka serikali ifuate sheria na kuwawekea wafugaji mipango mizuri ya ufugaji kwani sasa hali mbaya, wafugaji wanaokamatwa ndani ya hifadhi wanaonewa ikiwemo kubakwa. Mbunge wa Monduli, Kalanga Laizer (Chadema) alisema uuzwaji wa mifugo kiholela unawasababishia wafugaji umasikini. Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) alimwomba Waziri Maghembe asiache maofisa wake kuendelea kutaifisha mifugo.
Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM) alisema tatizo la mifugo ni kubwa na hatua ya wafugaji hao kuhamahama ndio chanzo cha maeneo ya wakulima kupata matatizo. “Watu wanalia kila kukicha mazao yao yameliwa na mifugo,” alisema. Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM) alisema wapiga kura wake wameshindwa kulima sababu ya wafugaji na kutaka kutengewa maeneo ya wafugaji na wakulima ili haki iweze kutendeka kwa wote.
Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (CUF) alisema wafugaji wengine ni majangili kwani wanaingia kwenye hifadhi na silaha hivyo wachunguzwe. Maghembe aliwaagiza wafanyakazi walio chini yake kupitia Katibu Mkuu hiyo kusimamisha utaratibu wa kupiga minada mifugo ya wafugaji hadi wizara itakapokwenda maeneo hayo kuchunguza tuhuma zilizotolewa.
KWAMATANGAZO YA BIASHARA TUPIGIE 0623372368
Chapisha Maoni