MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola amesema watendaji wote wanaodaiwa kuhusika katika sakata la kuzembea kudhibiti biashara ya kusafirisha mchanga wa dhahabu nje ya nchi, watachunguzwa na taasisi yake.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mlowola alisema hata watendaji ambao walihusika kwenye sakata hilo na sasa hivi hawapo madarakani au wanashikilia nyadhifa nyingine, nao lazima watahojiwa na taasisi hiyo ili kufahamu sababu ya kuruhusu taifa kupata hasara kubwa kiasi hicho. Watendaji hao ni wanaofanya kazi Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), Wizara ya Nishati na Madini na taasisi nyingine zinazohusika na madini.
“Kosa la jinai halina muda wala ukomo, wale ambao walikuwepo wizarani kitengo cha madini na kwa sasa hawapo nao tutawafuatilia,” alisema. Alisema taasisi yake itashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuchunguza suala hilo na watakaobainika kuhusika wote watashitakiwa. Mlowola alisema wameshaanza kazi waliyopewa na Rais kuwachunguza baadhi ya watumishi wa TMAA.
“Maelekezo ya Rais yalikuwa wazi kabisa kwetu na sisi tumeshaanza uchunguzi wetu,” alifafanua Mlowola. Pamoja na kutotaka kuingia kwa undani kuhusu uchunguzi wao, taarifa kutoka ndani ya TMAA zilisema Mtendaji Mkuu wa TMAA ambaye amesimamishwa kazi, Dominic Rwekaza jana aliripoti Takukuru. “CEO hayupo ofisini, taarifa tulizo nazo yuko Takukuru,” alisema mmoja wa wasaidizi wake ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi ambao hawakutaka kutajwa majina, walishangazwa na ripoti ya kamati maalum ya Rais juu ya ofisi za TMAA. Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alisema Rais Magufuli anaipenda nchi yake, angependa kila mwananchi afaidike na rasilimali za nchi lakini inaonekana baadhi ya watendaji ambao wamepewa majukumu ya kusimamia na kulinda rasilimali hizo, wanaangalia maslahi binafsi. Kuhusu kuunda kikosi kazi cha kushughulikia ulinzi wa rasilimali za nchi ikiwemo madini, Jenerali Mabeyo alisema tayari kipo na kinafanya kazi.
“Ila vyombo vya dola havipo kila eneo, tunachoomba kila mwananchi atusaidie kutupa taarifa za kiusalama,” alieleza Mkuu huyo wa JWTZ. Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema wameshaanza kutekeleza kazi waliyopewa na Rais Magufuli kuhusu ulinzi na kama kuna taarifa ambayo itahitajika kutolewa kwa umma watafanya hivyo. “Kwa sasa tunaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais,” alieleza Bulimba.
Baada ya kupokea ripoti ya ‘mchanga wa dhahabu’, Rais Magufuli aliagiza vyombo vya dola kuwachunguza Mtendaji Mkuu wa TMAA, Rwekaza na watendaji wengine wanaohusika na eneo hilo la usafirishaji makinikia Rais pia aliamuru watendaji wengine wachunguzwe na watakaobainika wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria kujibu tuhuma za kuipa hasara Serikali.
Rais pia alitengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa kushindwa kuisimamia TMAA na kutoonesha juhudi za kujenga kinu cha kuchenjulia mchanga wenye mchanganyiko wa madini licha ya kuagizwa na sera ya madini ya mwaka 2009 tangu mwaka 2010.
KWAMATANGAZO YA BIASHARA NYIMBO;TUPIGIE 0623372368
Chapisha Maoni