Simba juzi ilitumia dakika 120, kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho msimu ujao, baada ya kuifunga Mbao FC mabao 2-1, katika mchezo wa fainali ya michuano ya FA kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Akizungumza na gazeti hili Omog, alisema wachezaji wake walicheza kwa juhudi kubwa muda wote wa mchezo ndiyo maana wakapata ushindi huo na kutimiza malengo yao kwa kutwaa taji hilo. “Nawapongeza sana wachezaji wangu walicheza kwa nidhamu na kujituma muda wote wa mchezo, na hiyo inatokana na mikakati tuliyokuwa tumejiwekea ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kukosa taji la Ligi Kuu Bara,” alisema Omog.
Kocha huyo raia wa Cameroon pia hakusita kuwapongeza wapinzani wao Mbao FC, kwa kuonesha ushindani wa kweli na kusema walistahili kucheza fainali. Kwa upande wake kocha wa Mbao, Mrundi, Etienne Ndayariagije alizungumzia masikitiko yake dhidi ya mwamuzi aliyechezesha mpambano huo kuwa hakuwatendea haki, baada ya kuwapa Simba penalti isiyokuwa halali.
Ndyariagije alisema kwa sheria za Shirikisho la Soka wanakubali kuwa wamefungwa, lakini wao binafsi wanajua kuwa ndiyo mabingwa wa taji hilo, kwani walistaili kutokana na kiwago bora walichokionesha na kuwabana miamba hiyo ya soka nchini “Mwamuzi alijitahidi sana,lakini mwishoni alibadilika na kutoa maamuzi ambayo ni wazi yalionesha kuibeba Simba, hiyo haipendezi kwa sababu lengo siyo ubingwa lakini pia uwezo wa timu ili huko inapokwenda ikatuwakilishe vizuri,” alisema Ndyariagije.
Simba bado ipo Dodoma na leo inatarajiwa kulipeleka kombe hilo Bungeni, kufuatia mwaliko waliopewa na wabunge wanaoishabikia timu hiyo na baada ya hapo uongozi utatoa taarifa kuhusu kitakachofuata kama kurudi Dar es Salaam au kwingineko.
Chapisha Maoni