KAMATI maalum iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza kilicho kwenye makanikia maarufu kama mchanga wa dhahabu imebaini kuwemo kiasi kikubwa cha dhahabu na madini mengine tofauti na ilivyokuwa inadaiwa na kampuni zinazosafirisha mchanga na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).
Kwa mfano, madini yaliyo kwenye makontena 277 ya mchanga yaliyoko bandarini yalizuiwa na Serikali kusafirishwa nje ya nchi hadi ijiridhishe na kiwango cha madini kilichomo kwenye mchanga huo yana thamani kati ya Sh bilioni 829.4 na Sh trilioni 1.439.
Makontena hayo yalikuwa mali ya mgodi wa Buzwagi. Uchunguzi ulihusisha makampuni mengine ya dhahabu. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdukadir Mruma akiwasilisha ripoti yake jana alisema wenye migodi na (TMAA) walikuwa wanatoa takwimu za uongo jambo ambalo limeikosesha serikali mabilioni ya fedha kwa miaka 17 tangu biashara ya kusafirisha mchanga huo nje ianze.
“Tumebaini kuwepo kwa viwango vya juu vya dhahabu, shaba, fedha na madini mengine mengi,” alisema Profesa Mruma katika ripoti. Profesa Mruma alisema katika dhahabu walibaini kuwa kontena moja lenye tani 20 lina dhahabu kati ya gramu 671 na gramu 2,373. Kiasi hicho ni kati ya kilo 28 na kilo 47.5 ya dhahabu. Alisema kwa kontena 277 zilizokuwa zimezuiwa bandarini, kuna tani 7.8 zenye thamani ya Sh bilioni 676 hadi Sh trilioni 1.146.
Wakati kamati inabaini uwepo wa kiwango hicho, TMAA inaonyesha katika ripoti zake kuwa mchanga huo ulikuwa na gramu 200 sawa na kilo 4, na tani 1.2 za dhahabu. Alisema TMAA inaonesha makontena ya bandarini yana thamani ya Sh bilioni 97.5.
“Kiasi kilichokuwa kinatolewa na TMAA na wasafirishaji ni kidogo sana, uhalisia ni kwamba makontena yale yana dhahabu ya thamani ya Sh bilioni 676 kwa kiwango cha wastani na kiwango cha juu dhahabu ile ina thamani ya Sh trilioni 1.146,’’ alisema Profesa Mruma.
Alisema kwa takwimu hizo ni wazi kuwa udanganyifu huo unaofanywa katika sekta hiyo, umeikosesha Serikali mapato mengi hasa kupitia makusanyo ya mrabaha tangu uanze.
Kwa upande wa madini ya shaba, Profesa Mruma alisema huko nako kuna kiasi kikubwa cha shaba tofauti na takwimu za TMAA. Alisema kwa kila kontena, kuna shaba kati ya gramu 15.09 na gramu 33.78 kiasi ambacho wastani wake ni gramu 26 kwa tani.
Kiasi hicho ni sawa na tani kati ya 5 na 6 kwa kila kontena. Alisema makontena 277 yaliyozuiwa yalikuwa na uzito wa kilo 1,440 za shaba ambazo thamani yake ni Sh bilioni 17.9 hadi Sh bilioni 23. Profesa Mruma alisema katika hesabu zao, TMAA walikuwa wanadai kila kontena lina tani 4 ambazo thamani yake ni Sh bilioni 13. “Hapa kuna tofauti kubwa ya uzito na thamani ya madini.”
Profesa Mruma alisema kwa upande wa madini ya fedha walibaini kuwepo kwa gramu kati ya 202 na 351 ambazo ni wastani wa gramu 305. Alisema kiasi hicho ni kati ya kilo 6.1 na kilo 7.0 kwa kila kontena na kwa makontena 277, kulikuwa na kilo 1,689 ambazo ni sawa na tani 1.7.
Thamani ya madini hayo ni Sh bilioni 2.1. Alisema takwimu ambazo TMAA ilikuwa inatoa zinaonesha kwa kila kontena kulikuwa na kilo 3 kiwango ambacho ni nusu ya kile walichobaini.
Licha ya madini hayo, Profesa Mruma alisema pia kuwa kwenye mchanga huo kuna madini ya chuma ambayo ni kati ya gramu 13.3 na gramu 30.6 ambazo ni wastani wa gramu 27 kwa tani.
Alisema kiasi hicho ni tani kati ya 5.4 na tani 6.1 hivyo kwa makontena yote kuna uzito wa kilo 1,496 yenye thamani ya fedha ya Sh bilioni 2.3. Madini mengine ambayo yametajwa kuwa yamo kwenye mchanga huo ni Sulphur ambayo ni kati ya gramu 7.8 na gramu 10.2.
Mwenyekiti huyo alisema makontena 277 yalikuwa na uzito kati ya kilo 2,161 na kilo 2, 844 ya thamani ya Sh bilioni 1.4 na Sh bilioni 1.9. Alisema mchanga huo pia una madini mengine maarufu kama madini mkakati ambayo katika kila kontena kuna uzito wa kilo 6.4 na 13.75. Alisema yale makontena 277 bandarini yalikuwa na uzito wa kilo 1,773 na thamani yake ni kati ya Sh bilioni 108 na Sh bilioni 231.
“Kwenye ule mchanga kuna madini mengine mengi tu ambayo pia wasafirishaji walikuwa wanayauza. Thamani yote ya madini mkakati kwa makontena yaliyokuwa bandarini yalikuwa ni kati ya Sh bilioni 129.3 na bilioni 261.5. “Madini haya TMAA imekuwa haiyarekodi, hivyo hayajulikani lakini kuna kiasi kikubwa cha madini haya kwenye makanikia, huu ni upotevu mkubwa wa fedha za serikali,” alisema Mruma.
Uzito na utepe wa makontena Profesa Mruma alisema katika uchunguzi wao, wamebaini baadhi ya makotena yana uzito mkubwa tofauti na uzito wa kawaida, tani 20. Alitoa mfano kuwepo kwa makontena manne yaliyozidi uzito.
Alisema moja lilizidi uzito wa tani 3.1, lingine tani 2.95, moja kwa tani 2.7 na lingine uzito wake ulizidi kwa tani 2.2. Mwenyekiti huyo alisema kutokana na baadhi ya makontena kuwa na uzito mkubwa, ni wazi kuwa hata uzito wa madini pia utaongezeka.
Profesa Mruma pia alisema walifanya uchunguzi kwenye makontena mengine ya mchanga wa shaba yanayosafirishwa na wachimbaji wadogo kwenda nje pia. Alisema kwenye mchanga huo pia wamebaini kuwepo kwa dhahabu tofauti na inavyodaiwa na wachimbaji hao wadogo kuwa kwenye mchanga ule kukulikuwa na madini ya shaba tu. Alisema kwa kila tani walibaini kuwepo gramu 38.3 na akaomba Serikali iyaangalie makontena hayo ili iweze kupata mapato halisi yaliyopo.
“Pia kufahamika kwa madini haya kutawasaidia wachimbaji wadogo wanaosafirisha mchanga huo kufahamu kilichomo kwenye mchanga huo na kuboresha biashara na mapato,” alisema. Pia Profesa Mruma alisema udhibiti wa TMAA katika makontena ya mchanga ni mdogo kwani hawafungi na lakiri wanapomaliza kuchukua sampuli za mchanga ili kuzipima maabara.
“Hawa tumebaini kuwa wanapoenda kuchukua sampuli, lile kontena hawalifungi na utepe (lakiri), jambo linatoa mwanya kwa wawekezaji kufanya hujuma zozote ikiwa ni pamoja na kuongeza mchanga au kuficha madini,” alisema. Skana ya TPA haifanyi kazi Profesa Mruma alisema skana ya bandarini ambayo inatumiwa kuangalia bidhaa zilizoko kwenye makontena haionyeshi uhalisia wa vitu.
Alitoa mfano kuwa katika uchunguzi wao walikata vipande vya chuma kadhaa na kuviweka kwenye kontena ambalo lilikuwa na mchanga na kulipitisha kwenye skana hiyo ili kubaini kama mitambo hiyo inaonesha au la. “Ile skana haikuonesha vile vyuma, tulistaajabu maana kumbe watu wanaweza kupitisha bonge la dhahabu kwenye mchanga na skana ising’amue kuwepo kwa bonge hilo,” alisema.
Kamati yapendekeza timuatimua Profesa Mruma baada ya kuonesha uhalisia wa kilichomo kwenye mchanga huo, alipendekeza Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu watendaji wa TMAA na Wizara ya Nishati na Madini waliohusika kuikosesha Serikali mapato. Pia imeshauri Serikali iendelee kusitisha usafirishaji wa mchanga hadi hapo wasafirishaji watakapolipa mrabaha kwa kuangalia thamani halisi ya madini yaliyoko kwenye mchanga huo.
Wameshauri kujengwa kinu cha kuchenjulia mchanga huo nchini ili kutoa fursa nchi kujua madini halisi yaliyo katika makanikia hayo. Mapendekezo mengine ni kuitaka TMAA iwe inafunga lakiri makontena kila inapomaliza kuchukua sampuli ya mchanga na ipime aina zote za madini zinazopatikana kwenye mchanga huo ili serikali iweze kupata kodi yake stahiki. Pendekezo lao lingine ni kununua skana mpya itakayosaidia Serikali kutambua kilicho kwenye mizigo inayopitishwa bandari ya Dar es Salaam.
Wajumbe wa kamati Wajumbe wa kamati hiyo mbali na Profesa Mruma walikuwa ni Profesa Justianian Ikingula, Profesa Joseph Bushweshaiga, Dk Yusuf Ngenya, Dk Joseph Philip, Dk Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery Gombela.
Wengi ni wataalamu wa jiolojia na kemia na wengi walitoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Miongoni mwa hadidu za rejea walizokabidhiwa ni kuchunguza aina ya madini, kiasi na viwango vya madini katika mchanga unaosafirishwa na kampuni zinazochimba dhahabu nchini. Mchanga huo unapelekwa nje ya nchi kuchenjuliwa ili kupata madini yaliyobaki.
KAMA UNAMATANGAZO YA BIASHARA HABARI TUPIGIE SASA 0623372368






Chapisha Maoni