WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema nyumba zilizo kati ya mita 22.5 na 30.0 kila upande wa barabara zitalipwa fidia bomoa bomoa ikifanyika.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Edwin Ngonyani alisema fedha za kulipa fidia nyumba hizo zilizowekwa alama ya X ya kijani zinatolewa pamoja na bajeti ya ujenzi wa barabara husika unapoanza kufanyika. Alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM), aliyetaka kujua ni lini serikali itawalipa watu waliowekewa alama za X barabara ya Mkuranga - Kisiju.
Katika swali la msingi Ulega alitaka kujua kama serikali ipo tayari kuwalipa fidia. Ngonyani alisema, nyumba ambazo zimo kati ya mita 22.5 na 30 kila upande, wamiliki wake wanastahili kulipwa fidia. Alisema kwa sasa wananchi hao hawatakiwi kuendeleza chochote katika eneo hilo ingawa hawalazimiki kuondoa mali zao mpaka hapo serikali itakapohitaji eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Ngonyani alisema kabla serikali haijatwaa eneo hilo, uthamini utafanyika na wananchi wanaostahili kupewa fidia watalipwa. Alisema kulingana na Sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2007, eneo la hifadhi limeongezeka kutoka mita 22.5 hadi 30. “Barabara ya Mkuranga-Kisiju yenye urefu wa kilometa 46 ni miongoni mwa barabara zilizo chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads),” alisema.
Pia alisema, lengo la kuweka alama ya X ni kuwajulisha na kuwatahadharisha wananchi kuhusu ongezeko la eneo la hifadhi ya barabara ili wasiendeleze maeneo hayo. Nyumba zilizowekwa alama ya X nyingine zimejengwa katika hifadhi ya barabara ya mita 22.5 kila upande na wamiliki wake walipewa notisi ya kuziondoa bila kulipwa fidia kwani walivamia hifadhi ya barabara.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top