SERIKALI imekamata viuatilifu lita 14,600 vilivyokuwa chini ya viwango na visivyo na ubora vilivyokuwa vikipita njia za panya. Hayo yamesemwa jana Bungeni, Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Umwagiliaji, William Ole Nasha.
Alikuwa akitoa takwimu hizo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Sikudhani Chikambo (CCM). Chikambo alitaka kujua hatua gani zimechukuliwa na serikali dhidi ya kampuni zinazoingiza viuatilifu visivyofaa sokoni.
Nasha alisema, serikali huchukua hatua kali kwa kampuni zinazosambaza dawa na viuatilifu vilivyo chini ya viwango, ikiwa ni pamoja na kuzifungia na kuzifutia leseni. “Baadhi ya maduka yaliyokuwa yakiuza dawa na viuatilifu bandia, vilivyo chini ya viwango na visivyo na ubora, yamefungwa na kufutiwa leseni na mengine kesi zake zinaendelea mahakamani,” alisema Nasha.
Akijibu swali la msingi la Mbunge Chikambo aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani kudhibiti dawa zisizokidhi vigezo alisema imeweka mikakati kudhidhibiti kuingizwa. Nasha alisema udhibiti wa ubora na usalama wa dawa na viuatilifu vinavyoingia nchini na vilivyo sokoni unafanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa upande wa dawa za mifugo na Taasisi ya Utafiti Viuatilifu vya Kitropiki (TPRI) kwa viuatilifu.
Nasha alisema, taasisi hizo zimeweka mfumo wa usajili wa dawa zinazoingia nchini hivyo dawa na viuatilifu vinavyoingia lazima zisajiliwe ili kujiridhisha ubora, usalama na ufanisi kabla ya kuingia sokoni. Alisema pamoja na kuwa bei za dawa na viuatilifu zinapangwa na nguvu ya soko, serikali imeondoa ushuru wa forodha na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili kumpunguzia mkulima, mzigo wa bei. Alisema serikali inaendelea kupitia tozo na ada mbalimbali katika sekta ya kilimo kuona kama inafaa kuondolewa kumwongezea unafuu mkulima anayetumia dawa hizo
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top