UWEPO wa vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali ni ishara ya kusimamia usalama katika maeneo hayo na wananchi wanaamini kuwa polisi wapo katika maeneo hayo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
Kwa mujibu wa Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO) vituo hivyo vilianzishwa kwa ajili ya kuhakikisha usalama katika eneo kilipo kituo cha polisi na pia usalama wa wananchi wanaokizunguka. Hivyo ni muhimu kwa askari wanaopangiwa katika vituo hivyo kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Nimeanza kwa kuyasema hayo kutokana na tukio nililolishuhudia siku ya Jumapili katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo.
Siku ya Jumapili nilifika katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi Ubungo kwa ajili ya kupokea mzigo, nikiwa katika kituo hicho nilimshuhudia kijana mmoja sikupata uhakika kama alikuwa na akili timamu au ni mlevi, alikuwa amebeba chupa tupu za vilevi vikali na alikuwa anazivunja katika baraza za ofisi za mabasi kituoni hapo pamoja na kuwarushia watu waliokuwa wamesimama.
Kitendo hicho kilisababisha taharuki kwa wananchi waliokuwepo katika kituo hicho pamoja na watu waliokuwa katika ofisi zao na kusababisha watu hao kukimbia hovyo huku wengine wakikimbilia ndani ya ofisi hizo, jambo ambalo lingeweza kusababisha uharibifu wa mali.
Ndani ya kituo hicho kipo kituo cha polisi, baada ya tukio hilo niliamini polisi wangeweza kumtuliza kijana huyo ambaye alizua taharuki kubwa lakini polisi waliendelea kukaa ndani ya kituo hicho bila kufanya chochote.
Iliwalazimu vijana waliokuwepo katika kituo hicho kutafuta namna ya kuweza kumdhibiti kijana huyo na kila walipojaribu aliendelea kurusha chupa na kusababisha watu kurudi wakihofia kudhuriwa na chupa hizo.
Hali hiyo ilisababisha watu waliokuwa wamepaki magari katika eneo hilo kuanza kuyatoa magari hayo bila utaratibu wakihofia magari yao kupasuliwa vioo, kitendo cha kuondoa magari hayo bila utaratibu kingeweza kusababisha kugongwa kwa watu wanaokimbia.
Baada ya kuendelea kupasua chupa hizo alitokea kijana mmoja aliyejitoa mhanga kumkamata kijana huyo, jambo ambalo bado halikuwa salama kwa kuwa angeweza kudhurika na chupa alizokuwa akitupa yule kijana.
Kijana aliyejitoa kumkamata kijana huyo alifanikiwa, ndipo waliokuwa wakikimbia wakaenda kumkamata kijana huyo na kuanza kumshambulia huku wakielekea kituo cha polisi, lakini bado polisi walikuwa kimya hata wakati kijana huyo akipigwa.
Mwito wangu kwa polisi katika kituo hicho ni vyema wakawa sehemu ya kudhibiti matukio kama hayo ili kuhakikisha wanadhibiti athari ambazo zinaweza kutokea wakati wa tukio kama hilo.
Kijana yule angeweza kuumiza watu na kuleta madhara, kitendo cha polisi kukaa kimya pia kingeweza kusababisha kijana yule kupigwa hata kusababisha kuuwawa. Ombi langu kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Simon Sirro uangalie upya askari wako waliopo Ubungo na ikiwezekana waondoe maana wameshindwa kazi, walete wenye moyo na ari ya kazi.
KAMA UNAMATANGAZO YA BIASHARA NYIMBO ZA ASILI NK,WASILIANA NASI KUPITIA ..0623372368
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top