CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uhalifu unaoendelea kutokea wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani unatosha na kuitaka vyombo vya ulinzi na usalama kulichukulia suala hilo kwa uzito likome.
Kimesema yeyote mwenye dhamana na suala hilo ajitafakari kwani chama hicho kinahitaji watu wa maeneo hayo kurejeshewa imani na amani. Maeneo hayo yamekumbwa na mauaji mfululizo ya viongozi wa CCM. Katibu wa Sekretarieti, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia suala hilo.
Alisema CCM imekuwa inafuatilia kinachoendelea katika maeneo hayo na kujiridhisha kuwa kuna haja ya Serikali na vyombo vya ulinzi kuongeza umahiri, ubunifu na weledi wa kushughulia uhalifu huo ili usiendelee. “Tunatoa rai kubwa kwa serikali, tumevumilia, tumekaa kimya na kufuatilia sana suala hili, Watanzania wanakufa, tunataka kuona kitu kinatokea chenye kurudisha amani na hata imani kwa wananchi,” alisema Polepole.
Alisema wananchi wa maeneo hayo wanaishi kwa hofu huku wengine wakikimbia nyumba zao ilhali ni haohao waliomchagua Rais John Magufuli, hivyo wana haki ya kuwa na maisha yenye amani kila siku. Alisema kama suala hilo ni ujambazi au ujangili inatosha na ifikie mwisho kwani hiyo ni moja ya namna nyingine kuhujumu wananchi na mali zao. Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vishirikiane kurejesha amani, ili uchaguzi wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwaka huu ufanyike salama.
“Kazi ya chama madhubuti ni kuwasemea watu, wapo waliouawa kikatili na watu wasio na mioyo, hisia wala utu wakati hakuna dini inayoamini katika kutoa uhai wa mtu isipokuwa Mungu pekee,” alisema Polepole. Alituma salamu za pole kwa wote walioathirika na uhalifu huo wakiwemo viongozi na wanachama wa chama hicho ambao wamepoteza uhai.
KWAMATANGAZO YA BIASHARA NYIMBO TUPIGIE 0623372368
Chapisha Maoni