BENKI ya Dunia kupitia washirika wake wa maendeleo imesema imeridhishwa na hatua kubwa iliyochukuliwa na jamii ya wananchi wa Visiwa vya Zanzibar katika kusimamia miradi yao kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu katika kujiondolea umaskini.
Viongozi wa ujumbe wa washirika hao wa maendeleo ulitoa kauli hiyo wakati ukitoa tathmini ndogo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua miradi ya jamii inayotekelezwa kupitia Tasaf katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini Unguja na Pemba.
Kiongozi wa ujumbe huo kutoka Benki ya Dunia, Moderes Abdulah alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ziara yao imeshuhudia maendeleo makubwa yaliyopatikana katika Jamii kutokana na kundi kubwa la wananchi lilivyoamua kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi yao waliyoianzisha.
Moderes alisema Zanzibar imeonesha mfano bora katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia Tasaf awamu ya tatu kiasi kwamba uongozi wa Benki ya Dunia kupitia washirika wake imefurahia hatua hiyo ya mafanikio. Alifahamisha kwamba Benki ya Dunia kupitia washirika wake imeamua kuunga mkono miradi ya maendeleo kwa wananchi maskini katika nchi zinazoendelea ikilenga kuona ufanisi wa kudumu unapatikana katika kustawisha maisha yao ya kila siku.
Wakitoa ufafanuzi zaidi wa ziara hiyo ya kukagua miradi ya Tasaf visiwani Zanzibar, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislas Mwamanga na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Watoto (Unicef), Paul Quarles walisema upo ushahidi wa fedha zinazotolewa na Tasaf kutumika katika utaratibu maalumu uliowekwa.
Walisema ujenzi wa nyumba za kudumu, upatikanaji wa sare za skuli, uanzishwaji wa Vitalu vya miti ya kudumu, ujenzi wa majengo ya shule na madrasa kwa kaya maskini ni mfano wa matumizi hayo sahihi ya fedha hizo. Wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa usimamizi wake mzuri kwenye miradi ya mfuko huo wa Tasaf.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Chapisha Maoni

 
Top